WAKULIMA TUNDURU WAILALAMIKIA SERIKALI KWA KUWEKA MZABUNI MMOJA TU WA KUSAMBAZA PEMBEJEO KWA ZAO LA KOROSHO
Na Joseph Mwambije
Tunduru
Wakulima wa zao la Korosho wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wamelalamikia kitendo cha serikali kuweka mzabuni mmoja tu anayesambaza pembejeo kwa wakulima wote wa zao hilo nchini, hali inayosababisha ashindwe kuhudumia maeneo yote kwa uhakika.
Tunduru
Wakulima wa zao la Korosho wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wamelalamikia kitendo cha serikali kuweka mzabuni mmoja tu anayesambaza pembejeo kwa wakulima wote wa zao hilo nchini, hali inayosababisha ashindwe kuhudumia maeneo yote kwa uhakika.
Wakizungumza mjini Tunduru juzi wakulima
hao wakiwemo wanachama wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA), walisema
kuwa hali hiyo ya kuwa na wakala mmoja imekuwa ikisababisha ucheleweshaji wa
pembejeo za ruzuku mapema kulingana na msimu.
“Katika wilaya yetu hii zao kubwa
tunalotegemea ni korosho, kwa mwaka huu tuliaambiwa sumu ya kuua wadudu aina sulpher
itapatikana kwa muda muafaka ambao ni mwezi wa sita miti inapoanza kutoa maua
na itauzwa shilingi 12,000 na itaenda kuchukuliwa Mtwara lakini cha kushangaza
wakala tunayemtegeme huku alienda mkoani Mtwara na magari yake na kurudi bila
sulpher hiyo kwa maelezo kuwa imekwisha,” walisema wakulima hao.
Wamesema kuwa kwa sasa wanatumia gharama kubwa kununua
sulpher ili kupulizia maua
ya korosho yasianguke, badala ya kutumia shilingi 12,000 kununua kwa bei ya
ruzuku sumu hiyo sasa wanainunua kwenye maduka ya kawaida kwa shilingi 50,000 gharama
ambayo ni kubwa ukilinganisha na bei ya korosho.
Bw. Ali Msanjo mkulima mdogo wa Korosho wilaya
ya Tunduru ambaye pia ni mwanachama wa Mtandao wa Vikundi Vya Wakulima Tanzania
(MVIWATA) na ambaye pia ni mdau wa bodi ya korosho Tanzania alisema kikao cha
Bodi ya Korosho kilichofanyika Tanga kilikubaliana kuwa asilimia 65 ya mauzo ya
korosho itarudi Halmashauri ili kuwezesha kupata pembejeo ya ruzuku kwa wakati
lakini wakulima wanashanga makubaliano hayo hayajatekelezwa.
Naye Bw. Rashidi Masudi mkulima wa Korosho
alisema kinachomshangaza kwa sasa ni kuona wakala waliyekuwa wakimtegemea awauzie
pembejeo za ruzuku ya Sulpher kwa sasa anauza dawa hiyo ya sulpher kwa bei isiyokuwa
ya ruzuku ya shilingi 35,000 tofauti na wafanyabiashara wengine wanaouza kwa
Shilingi 50, 000, jambo ambalo linawapa wasiwasi wakulima kwamba huenda kuna
mchezo mchafu umefanyika ili kudhulumu haki yao.
Kwa upande wake Afisa Pembejeo wa wilaya ya Tunduru Bw. Hassan Simba alisema kuwa wakala wa awali
aliyekuwa amekabidhiwa jukumu la kusambaza pembejeo hizo aligundulika kuwa ni
mdanganyifu na kwamba hatua za kumuondoa zimeshachukuliwa na wakala mpya
ameshapatikana.
Afisa pembejeo huyo aliongeza kwa sasa wameamua kufanya juhudi binafsi ili kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo kwa wakati na kwamba kwa kushauriana na Mkuu wa Wilaya wamefanikiwa kupata tani 50 tu toka kwa msambazaji tofauti na yule anayetegemewa na bodi ya korosho. Alisema kiasi hicho cha tano 50 ndicho kinauzwa kwa shilingi 35,000 badala ya Sh.50, 000 baada ya serikali wilayaguzia wakulima gharama.
No comments:
Post a Comment