AJALI YA BOTI ZANZIBAR:Gunia liliniokoa
AJALI YA BOTI ZANZIBAR:Gunia liliniokoa |
Mwambinge ambaye amelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar alisema: “Sijui kuogelea, lakini nilikaa kwenye maji kwa saa nne. Nilichoka na kukakata tamaa, nikajiachia ili ikiwezekana nife, lakini nashangaa leo hii ni mzima.” Mtumishi huyo Tume ya Atomiki ambaye alikuwa safarini kuelekea Pemba kikazi, alisema aliokolewa akiwa hajitambui... “Ninachokumbuka ni kwamba waokoaji walinifunga kamba shingoni nikapata maumivu makali, nikapiga kelele wakaniachia, nikatumbukia tena kwenye maji na baadaye walifanikiwa kuniokoa na kuniweka kwenye boti.” Alisema wakati akiwa katika harakati za kujiokoa, aliwaona watu kadhaa wakiwa wamekufa wakiwamo watoto. Kwa upande wake, Ali alisema baada ya meli kuzama na yeye kutupwa nje, aliona gunia na kulidaka. Anasema alilishikilia kwa zaidi ya saa mbili kabla ya kuonwa na vikosi vya uokoaji. Abiria mwingine mkazi wa Bagamoyo, Hamisa Akida alisema meli hiyo ilizama ghafla na haikuwa rahisi kuwa na maandalizi ya kujiokoa: “Kwa jinsi meli hiyo ilivyozama ghafla haikuwa rahisi kujiokoa, kilichotokea hadi tukaokolewa ni mapenzi ya Mungu,” alisema. Alisema hali alipookolewa alikuwa ameshakunywa maji mengi na kuishiwa nguvu... “ lakini nashukuru ni mzima.” Waliopatikana jana Wakati majeruhi hao wakieleza hayo, jitihada za vikosi vya uokoaji hadi jana zilifanikisha kupatikana kwa miili 68 na kati ya hiyo 16 ilitambuliwa. Waliotambuliwa ni Husna Ali Hamis (34) na Kulthum Haji Khamis (34) wote wakazi wa Bagamoyo na Sichana Pandu (45 wa Kilimahewa Zanzibar). Wengine ni Nadra Maulid Mkubwa (17) wa Chumuni, Zanzibar, Mwanaidi Abdallah Ramadhani (21) wa Morogoro, Zubeda Jumanne Kwagaya (26- Meya), Idd Masoud Omari (Miezi 7- Tomondo) Riziki Mohamed Idd (21- Fuoni Zanzibar), Mwanaisha Khamis Haji (75) na Amina Shabani Kibega (24) wote wa Jang’ombe, Zanzibar. Pia wamo Laki Victor Kadoro (28- Mbagala, Dar es Salaam), Damas Leo Mlima (54- Shangani), Halima Sharifu Abdala (21-Kigamboni, Dar es Salaam), Ali Juma Ali (44- Jang’ombe, Zanzibar), Raya Ramadhani Hasani (2- Shakani) Mwanaisha Omari Juma (20- Bunju, Dar es Salaam) na Maryam Idd Omari Omari (25) Shakani. Washindwa kutambua miili Hali katika Viwanja vya Maisara, wanakohifadhiwa maiti jana kulikuwa na mkanganyiko baada ya wananchi wengi kushindwa kuwaona ndugu zao ambao walikuwa wamesafiri katika meli hiyo wakiwamo raia wa kigeni. Maiti moja ya raia wa Kenya imetambuliwa na ndugu zao ambao hata hivyo, walisema wamechanganyikiwa kuhusu namna ya kusafirisha mwili kwenda kwao. Mmoja wa ndugu, John Mumee alisema wameitambua maiti ya ndugu yao aitwaye Martina Masela... “Lakini hatujui tutaisafirisha vipi kwenda Mombasa kwa sababu hatuna fedha, lakini pia hatuelewi tutasafirisha kwa njia gani kwa sababu mashirika ya ndege hayataki kusafirisha maiti.” Alisema marehemu alikuwa akisafiri na mumewe, Bernard Kalii kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar wakiwa na ndugu mwingine, Mary Kioko ambao bado hawajapatikana. “Tumepata maiti hiyo moja lakini wenzake wawili bado hatujawapata, hatuelewi tufanye nini hapa tumechanganyikiwa tunaomba msaada wa haraka,” alisema Mumee. Waliiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuwasiliana na Ubalozi wa Kenya nchini ili kuona kama kuna uwezekano wa kuwasaidia kuisafirisha maiti hiyo ambayo alisema imeanza kuharibika. Mkazi wa Temeke, Dar es Salaam, Ali Mzee Moto alisema, hadi sasa hajawaona binti yake, Mwamini Ali aliyekuwa na mtoto wake mchanga. “Walisafiri na meli hiyo na walikuwa wakipitia Zanzibar ili siku inayofuata waende Pemba. Alikuwa anamfuata mchumba wake lakini Mungu hakupenda afike huko,” alisema Moto. Alishangazwa na shughuli ya uokoaji kusuasua na kuhoji sababu za Serikali kushindwa kuomba msaada wa waokoaji kutoka nje. “Tunafahamu ndugu zetu watakuwa wamekufa, lakini tunachoomba sisi ni kupata miili yao ili twende tukawazike,” alisema Moto. Mwingine aliyepotelewa na mtoto ni Philip Cassian John anayefanya kazi Trans Cargo, Dar es Salaam alisema, hajamwona mwanaye Thobias Joseph, anayefanya kazi katika Kampuni ya Hugo Domingo aliyesafiri na meli hiyo kwa safari za kikazi. “Walisafiri na wafanyakazi wenzake ambao maiti zao zimepatikana, sasa niko hapa kusubiri kati ya watakaookolewa leo kama nitamwona mwanangu.” Maiti zaharibika Kati ya maiti 68 zilizoopolewa baharini, 10 hazikutambuliwa na zilizikwa jana na SMZ katika makaburi ya Kama huko Bububu, Zanzibar. Mwenyekiti wa Kamati ya kushughulikia mazishi, Abdallah Twalib alisema maiti zimeharibika vibaya. “Hata baadhi ya ndugu waliozitambua maiti zao wameiomba Serikali izike kwenye makaburi ya eneo la Kama baada ya kuharibika vibaya,” alisema. Sijiuzulu ng’o Juzi, Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu wa Zanzibar, Hamad Masoud Hamad alisema hawezi kujiuzulu kwa tukio hilo kwa kuwa ni mapenzi ya Mungu. Hamad alisema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari akiwa na mawaziri wenzake wanne kutoka katika Serikali ya Muungano na wa SMZ. Hao walikuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Waziri wa Habari na Michezo wa SMZ, Ali Mbarouk na Waziri wa Katiba na Sheria SMZ, Aboubakar Hamis. Alipoulizwa kama ana mpango wa kujiuzulu kutokana na ajali hiyo ambayo ni ya pili kutokea katika kipindi cha mwaka mmoja, Hamad alisema: “Hivi ningezuiaje upepo usitokee? Ajali hii ni mapenzi ya Mungu kwani haiwezi kuzuiliwa na binadamu kwa sababu imetokana na upepo mkali na ilitokea ghafla, katika kipindi kisichozidi dakika tano meli ilikuwa imezama,” alisema Hamad. “Kujiuzulu siyo utatuzi wa tatizo, bali ni kumwomba Mungu atuepushe na majanga kama haya ambayo hayawezi kuzuiwa na binadamu.” Waziri huyo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa anayetokea Chama cha CUF alisema, kauli za kumtaka ajiuzulu ni mbinu chafu za kisiasa zinazofanywa dhidi yake ili aonekane hafai kuongoza. “Walinipiga vita hata kwenye ajali ya meli ya Mv Spice Islander wakitaka nijiuzulu lakini hata majibu ya tume iliyoundwa kuchunguza ilinisafisha kwamba sihusiki,” alisema. Dk Mwakyembe alisema Watanzania hawana sababu ya kumtafuta mchawi wa ajali hiyo kwani imetokea kwa bahati mbaya... “Tukubali kwamba ajali hii ni bahati mbaya. Maofisa wetu wametuthibitishia bila kuwa na shaka kwamba meli ilikuwa nzima na haikuzidisha abiria, kujiuzulu siyo suluhisho, tushikamane katika kipindi hiki kigumu.” Uzoefu wa mabaharia Mmoja wa mabaharia katika Kivuko cha Bandari ya Dar es Salaam, John Peter amesema Serikali inapaswa kulaumiwa kwa tukio hilo. Peter ambaye amekuwa baharia kwa miaka 24 sasa alisema, pamoja na Serikali kuwa na wataalamu wa kukagua vyombo hivyo kabla, ufisadi katika usajili wa meli bado ni tatizo. “Kama Marine Suveyer (Mtafiti wa Meli) angetekeleza majukumu yake, naamini tusingekuwa na meli mbovu kama hizi,” alisema. Baharia mwingine mwenye uzoefu wa miaka 40, maarufu kama Kepteni Magamba alisema anayepaswa kulaumiwa katika ajali hiyo ni kiongozi wa safari za meli. Kiongozi huyo (Port State Controller) hupokea taarifa kutoka mamlaka ya hali ya hewa na kuruhusu meli iondoke au isiondoke. Kiongozi huyo husimamia usalama wa meli ndani na nje ya bahari kwa kushirikiana na eneo meli inapoelekea. “Meli kabla ya kuondoka lazima ifuate taratibu zote, nahodha hupata kibali kutoka Sumatra (clearance) na kuipeleka kwa ‘Port State Controller’ ambaye tayari anakuwa ameshapata taarifa za hali ya hewa,” alisema Magamba. Wanasiasa Vyama kadhaa vya siasa vimetoa salamu za pole kwa wafiwa na kuishauri Serikali kuongeza umakini katika ukaguzi wa vyombo vya baharini. Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba aliitaka Serikali kuangalia upya uwajibikaji, utendaji na mwenendo wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) akidai kuwa taasisi hiyo imeshindwa kuwajibika ipasavyo kudhibiti vyombo vya usafiri. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa ameshauri kanuni za Bunge zinazotumika hivi sasa kuangaliwa upya ili kuruhusu Bunge kujadili ajali hiyo... “Nimesikitishwa na kitendo cha Naibu Spika (Job Ndugai) kuzuia wabunge kujadili suala la kuzama kwa meli bungeni kwa maelezo kuwa kanuni haziruhusu. Nitoe wito kwa kanuni kuangaliwa upya ili kuruhusu Bunge kujadili masuala ya kitaifa pindi yanapotokea.” Mwenyekiti wa APPT Maendeleo, Peter Mziray alisema: “Lipo tatizo katika uingizaji, ukaguzi na usajili wa vyombo vya usafirishaji wa majini… Serikali na mamlaka zinazohusika na usajili hazifanyi kazi kwa kuzingatia umuhimu wa kazi waliyopewa na matokeo yake ndiyo kuruhusu vyombo vibovu kubeba roho za watu.” Sumatra yajitetea Hata hivyo, Sumatra imejitetea kwamba haitambui usajili wa boti hiyo ya Mv Skagit. Meneja Uhusiano wa Sumatra, David Mziray alisema meli hiyo ilisajiliwa na Mamlaka ya Usafiri wa Majini Zanzibar (ZMA). Alisema meli hiyo ilipewa cheti cha ubora na mamlaka hiyo Agosti, 24 mwaka jana ambacho kinamalizika muda wake, Agosti 23, mwaka huu ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 300 na tani 26 za mizigo... “Hatuwezi kutoa maelezo zaidi kwa sababu ilisajiliwa Zanzibar na si huku kwetu.” Habari hii imeandikwa na Burhani Yakub, Pangani; Raymond Kaminyoge na Salma Said, Zanzibar; Kelvin Matandiko, Nora Damian, Joyce Mmasi, Geofrey Nyang’oro na Aidan Mhando Dar. |
No comments:
Post a Comment