Mama Kanumba, Flora Mtegoa.
Mama Lulu, Lucresia Karugila.
CHOKOCHOKO zimeanza! Huku kesi ya kifo cha mwanaye ikiendelea na Elizabeth Michael Kimemeta ‘Lulu’ akisota nyuma ya nondo za mahabusu ya Segerea, mama mzazi wa marehemu Steven Charles Kanumba ‘The Great’, Flora Mtegoa amemvaa mama Lulu, Lucresia Karugila, Ijumaa linafunguka.
MANENO MAZITO YA AIBU
Kwenye mahojiano maalum na gazeti hili nyumbani kwake Kimara-Temboni, Dar es Salaam, mapema Jumanne wiki hii, mama Kanumba alimtolea mama Lulu maneno mazito huku akimshangaa kwa kushindwa kumpa pole na kumfariji tangu mwanaye afikwe na umauti Aprili 7, mwaka huu.
Mama Kanumba alisema anaongea kwa uchungu kwani hakutegemea kama mama Lulu anaweza kuwa kimya mpaka leo hii bila hata kumpa pole wakati matatizo yamewakuta watoto wao wote.
TUPATE SAUTI YA MAMA KANUMBA
Ijumaa: Ili kupata kile alichokisema mzazi huyo mbele ya gazeti hili, tujiunge naye akiwa nyumbani kwake Kimara-Temboni.
Kwako mama Kanumba: Namshangaa sana mama Lulu kwani namuona kama siyo mzazi mwenzangu. Huwezi amini mpaka leo hii hajawahi hata kunipa pole wala kunitumia ujumbe wa watu kunifariji, hivi anategemea mimi nimfuate? Yeye mwanaye yupo hai wangu ndiyo ametangulia. Nimeona niseme kabisa nimpe habari yake.
Ijumaa: Kwani wewe uliwahi kufanya jitihada za kukutana na kufarijiana naye akakataa?
Mama Kanumba: Mama Lulu siyo kabisa. Aliwahi kufuatwa na kuombwa ushirikiano wakati kesi imefunguliwa akakataa.
Ijumaa: Mbona kuna madai kuwa baada ya kifo cha Kanumba upande wa Lulu ulikufuata ukakataa kutoa ushirikiano?
Mama Kanumba: Sijawahi kuongea na mtu yeyote wa upande wa Lulu. Huyo anayedai alikuja kuniomba ushirikiano nikamfukuza ananisingizia kwani simfahamu Lulu na mama yake zaidi ya kuwaona kwenye vyombo vya habari na filamu (Lulu).
Ijumaa: Je, akikufuata utamkubalia aje kukufariji?
Mama Kanumba: Mimi sina nia mbaya na mama Lulu, kibinadamu namuona kakosea kwani kama yeye alikuwa akiogopa, angetuma watu waje kwa niaba yake. Nilidhani alikuwa akiogopa kuja Sinza (Vatican kwa Kanumba) kwa sababu ya waandishi lakini hata nilipohamia huku (Temboni) hajaja. Ukweli ni kwamba akija nitampokea tu ila sidhani kama ipo siku atakuja, nawashangaa hata washauri wake.
Ijumaa: Unaizungumziaje filamu ya Foolish Age ya Lulu ambayo Kanumba aliipeleka Steps?
Mama Kanumba: Ni kweli filamu hiyo ipo Steps, Kanumba ndiye aliipeleka kwa nia ya kumuinua Lulu lakini kabla haijalipwa mauti yakamkuta. Ingekuwa ya Kanumba ningefuatilia.
Baada ya mahojiano hayo, Ijumaa lilitafuta mzani upande wa pili wa mama Lulu ambapo mahojiano yalikuwa hivi:
TUJIUNGE NA MAMA LULU AKIWA TABATA
Ijumaa: Mama Lulu gazeti la Ijumaa limezungumza na mama Kanumba anakulaumu kwa kushindwa kumfariji baada ya kifo cha mwanaye Kanumba aliyekutwa na umauti akiwa na Lulu. Je, unalizungumziaje suala hili?
Mama Lulu: Eehee unasemaje? Wewe ni nani? Mwandishi? Nimeshawaambia mniache kabisa kwani bila habari ya Lulu na Kanumba hamuuzi?
Ijumaa: Katika maadili ya kazi yetu mtu mmoja akiongea lolote juu ya mwenzake lazima pande zote zisikilizwe hivyo hii ndiyo nafasi yako. Unalizungumziaje suala hilo la mama Kanumba?
Mama Lulu: Sitaki kushauriwa na wewe mwandishi, nina washauri wazuri tu tena ni watu wazima, tafadhali naomba mniache nipumzike.
KIFUATACHO
Bado kesi ya Lulu ni mbichi ambapo itaendelea kuunguruma baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kumaliza utata wa umri na jina la Lulu Julai 23, mwaka huu.
KALAMU YA IJUMAA
Wazazi hawa wanapaswa kuwa na staha kwa sababu kila upande una machungu. Kanumba hatunaye na Lulu yupo nyuma ya nondo. Ni vyema wakakaa chini bila kukorogana ili kupunguza machungu waliyonayo.
No comments:
Post a Comment