FIKIWA WATU 63, SERIKALI YATANGAZA SIKU TATU MAOMBOLEZO | ||
JESHI
la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Omari Hassan
Mnkhon ambaye ni Meneja wa boti ya Mv Skagit, kwa ajili ya mahojiano
baada ya kubainika kwamba kumekuwa na kasoro za kumbukumbu katika
taarifa za hiyo.Wakati Jeshi hilo likimshikilia meneja huyo, hadi jana
jioni saa 10:30, vikosi vya uokoaji vilifanikiwa kupata maiti 63, huku
29 kati yao ikiwa imetambuliwa majina namba za tiketi na sehemu
wanakotoka marehemu. Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa meneja wa boti Mkoa wa Dar es Salaam, anashikiliwa ili kuweza kusaidia jeshi la polisi kupata taarifa za kina kuhusu za meli hiyo. Kova alisema tukio hilo linagusa maeneo mengi ikiwa ni pamoja na Mkoa wa Dar es Salaam ambako safari za meli hiyo huanzia na kuongeza kwamba, wanamshikilia meneje huyo baada ya kukosekana taarifa muhimu juu ya safari za boti hiyo. “Tunamshikilia meneja wa meneja hiyo ili atusaidie kutupa taarifa za kina, kwani tukio hilo sio dogo na uchunguzi wa kina unatakiwa kufanywa,” alisema Kova na kuongeza; “Jeshi la polisi litafanya uchunguzi wa kina kwa kushirikiana na vyombo na mamlaka zinazohusika, ili kujua chanzo cha ajali pamoja na kupata taarifa za kina za boti hiyo tangu ilipoanza safari yake,” alisema. Maiti zilizotambuliwa Hadi saa 10 jioni jana, maiti 63 zilikuwa zimepatikana na watu 145 kuokolewa wakiwa hai. Hata hivyo kati ya maiti hizo zilizopatikana, matiti 34 zilichukuliwa na ndugu zao. Baadhi ya maiti waliotambuliwa pamoja na umri wao na maeneo wanayoishi katika mabano ni Anita Emanuel (42, Kibamba -Dar es Salaam), Rukiya Issa Muombwa (miezi 2, Meli nne –Fuoni Zanzibar ), Halima Ali Khamis (23, Mtopepo- Zanzibar), Kolin Krispin (miezi 9, Kunduchi - Dares Salaam) na Rahma Ali Abdalla (miaka 52, Mfenesini - Zanzibar). Maiti wengine ni Said Jumanne Masanja (miaka 9, Nzega Tabora), Sauda Abdalla Omar (22, Ole Pemba), Said Juma Said (36, Arusha), Amina Abdalla Tindwa, (miezi 6, Fuoni), Halima Ramadhani Kilimo, (53, Morogoro), Khadija Omar Ali (58), Amina Hamir Bakari (39, Chukwani - Zanzibar), Mwanahamisi Mshauri (42, Kibandamaiti), Ali Hamdu Othman (35, Mkwajuni) na Mohamed Said Salum (40, Magomeni Mikumi - Dares Salaam). Wengine ni Amina Ahmed Ramadhani (21, Michenzani zanzibar ), Mgeni Juma Halfani (25, Daraja Bovu), Khadija Rajab Kibune (22, Fuoni), Maua Ramadhani Feruzi (29, Mwembeladu), Hussein Ali Khamis (4, Mwanakwerekwe) na Sabiha Heri Mbarouk (25, Mgeleme, Chakechake-Pemba). Pia wamo Halima Ali Mohamed (35, Kiwengwa- Zanzibar), Asia Juma Khamis (29, Kiembe Samaki), Yusuf Hasan Yusuf (7, Chamanzi, Dar es Salaam), Batuli Abrahmani Amir (20, Jang'ombe), Fatma Said Sultani (54, Msasani Dar es Salaam), Juma Jafari Shajak (Miezi 6, Kimaneta - Tanga) na Mohamed Ali Ngombe (41, Buguruni - Dares Salaam). Serikali yatangaza siku tatu za maombolezo Kufuatia msiba huo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetangaza siku tatu za maombolezo kuanzia Julai 19 hadi Julai 21 mwaka huu. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein alisema bendera zote zitapepea nusu mlingoti na shughuli zote zinazoambatana na sherehe na burudani zimefutwa kwa muda huo lakini kazi na shughuli za Serikali zitaendelea kama kawaida Nayo Serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi ilitangaza siku tatu za maombolezo kufuatia msiba huo mkubwa uliolikumba taifa. Lukuvi aliwaambia waandishi katika kipindi hicho cha siku tatu bendera zitapepea nusu mlingoti na shughuli za starehe zitasimamishwa ila kazi zitaendelea kama kawaida. Rais Shein amewahakikishia wananchi na hasa waliopoteza jamaa zao kuwa Serikali itabeba gharama zote za mazishi na huduma za matibabu kwa majeruhi. “Nimesikitishwa sana na msiba huu. Katika wakati huu si vema tukaanza kulaumiana jambo la muhimu hivi sasa ni kuokoa maisha ya watu,” alisema Rais Dk Shein. Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick alisema kutokana na maagizo ya Waziri Mkuu aliyoyatoa Bungeni Mkoa wa Dar es Salaam ndio umepewa jukumu la kushuhulikia suala hilo. Alisema kwa sasa mkoa Umepanga kutoa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kuhifadhi mili ya watu waliofariki katika ajali hiyo. “Tumepanga kwamba, Hospitali ya Taifa Muhimbili ndio itahusika katika kuhifadhi miili ya watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo,” alisema Sadick na kuongeza; “Watu wote ambao wanajua kuwa ndugu zao walisafiri na meli hiyo wafike katika bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya utambuzi,” alisema na kuongeza kuwa ambayo haitatambuliwa Serikali itachukua jukumu la kuizika. EU yatoa ndege ya uokoaji Katika kuonyesha kuguswa na ajali hiyo, Umoja wa Ulaya (EU) umetoa ndege maalum kusaidia juhudi za utafutaji na uokoaji katika eneo la ajali. Balozi wa Uingereza hapa nchini Diane Corner aliwaambia waandishi wa habari mjini Zanzibar kuwa wameamua kutoa msaada wa ndege hiyo ambayo iliwasaili Zanzibar usiku wa kuamkia Julai 19, kitokea katika visiwa vya Ushelisheli. “Hii ni ndege maalum ambayo kazi yake ni kuratibu na kubainisha eneo ambalo kuna watu na inawasiliana na waokoaji walioko majini ikiwa angani,” alisema Balozi Corner. Alifafanua kwamba, Umoja wa Ulaya unaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) katika kazi ya uokoaji, lakini pia Umoja huo upo tayari kutoa msaada wowote utaohitajika. Kwa upande wake, Balozi wa Marekani nchini, Leahant Alfonso alisema Serikali yake imetoa msaada wa dawa kwa ajili ya watu waliojeruhiwa katika ajali hiyo. Balozi Alfonso aliipongeza SMZ kwa kuchukua hatua haraka kukabiliana na maafa hayo. “Nawapa pole watu wa Zanzibar kwa msiba huu, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana, hasa nilipoziona maiti saba za watoto wadogo. Moyo wangu umeumia sana,” alisema huku akibubujikwa machozi. Wabunge wachangia maafa Katika hatua nyingine, wabunge wote watakatwa posho ya siku moja kuchangia maafa ya kuzama kwa boti hiyo huku Bunge likiahirishwa kwa siku moja kuomboleza maafa hayo. Posho hizo za wabunge zitawezesha kupatikana kwa Sh24.6 milioni kutoka kwa Wabunge wa sasa 352 ambao kila mmoja atachagia Sh70,000. Spika Anne Makinda jana asubuhi aliahirisha shughuli za Bunge kwa siku moja na kutangaza kuwa, Kamati ya Uongozi ya Bunge katika kikao chake jana asubuhi, iliamua zikatwe posho za siku moja na fedha hizo zitatolewa kama rambirambi kwa ndugu wa watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo. Wakizungumza baada ya ajali hiyo, baadhi ya wabunge waliitupia lawama Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), kwa kile walichodai kuwa ilishindwa kutoa taarifa ya tahadhari kwa watumiaji wa usafiri wa majini. Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde alisema mamlaka hiyo inabeba lawama kwa kushindwa kutoa ushauri kwa vyombo husika na badala yake wanafanya kazi ya kutabiri mvua tu. “Wale jamaa hawafai kabisa, matatizo yote wanatakiwa kubebeshwa wao kwa kuwa hawakuweza kutoa ushauri juu ya nini kingetokea mbele ya safari,’’ alisema Lusinde. Mbali na Mamlaka ya Hali ya hewa, lakini mbunge huyo alitaka pia wakaguzi wa vyombo vya majini kuwajibika kwa kushindwa kukagua uimara wa vyombo hivyo. Kwa upande wake Mbuge wa Viti Maalumu (CCM), Martha Mlata alisema tukio la kuzama kwa meli hiyo alilipokea kwa masikitiko lakini akasema “ni kazi ya Mungu.’’ Mlata alisema tangu juzi yeye pamoja na wabunge wengine wako katika maombi mazito ya kutaka Mungu awanusuru majeruhi na kuwapa nguvu ya ujasiri waokoaji ili wafanya kazi yao kwa moyo wa kujituma zaidi. “Unajua tunafanya mambo tangu tulipopata taarifa za ajali hiyo na hadi sasa tunatakiwa kuendelea kufanya maombi hayo kwa ajili yha ndugu zetu, naamini mkono wa Mungu hautapungukia kitu,’’alisema Mlata. Ushuhuda wa mabaharia, waokoaji Akizungumzia ajali hiyo, mmoja wa waokoajii binafsi, waliofika katika tukio hilo alisema boti hiyo imebinuka ikiwa mgongo juu. Mmoja wa wahanga aliyenusurika katika ajali hiyo, Hassan Khatib alisema tangu waliondoka Dar es Salaam mnamo saa 6:00 mchana juzi, hali ya bahari ilikuwa mbaya kwa sababu kulikuwa na mawimbi makubwa baadaye meli ilizidiwa na kupoteza mwelekeo. Alisema baada ya hapo ililala upande na kisha ilibinuka na yeye kutupwa kwenye maji na akawa hana kitu cha kushika ndipo alianza kuogelea na kufanikiwa kushi ubao na kuogelea nao. Alisema huduma uokoaji zilichelewa kufika ila mara baada ya ajali ilifika ndege na kuzunguka katika eneo la tukio na kuondoka na baada ya saa kadhaa vilifika vyombo ukoaji. TMA watoa kauli Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Dk Hamza Kabelwa alisema kuwa, kupitia ofisi yao iliyopo bandarini Dar es Salaam walitoa taarifa kwenye vyombo vya usafiri wa majini juu ya upepo mkali uliokuwa ukivuma baharini kwa kasi ya kilometa tatu kwa saa kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 5:00 asubuhi. “Tulipogundua hali hiyo tulitoa taarifa kwa wahusika wa vyombo vya usafiri wa majini tu,” alifafanua Dk Kabelwa. Meli ya Skagit ilitengenezwa mwaka 1989 nchini Marekani na ilikuja nchini 2008. Shahihisho Jana gazeti hili lilichapisha kwa makosa kuwa meli iliyozama inaitwa MvSkad badala ya Skagit. Habari hii imeandikwa na Boniface Meena, Habiel Chidawali, Dodoma, Salma Said, Zanzibar Aidan Mhando, Pamela Chilongola na Victoria Mhagama, Dar |
Friday, July 20, 2012
AJALI YA MELI ILITISHAKWELI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment