Monday, June 18, 2012

DOGO JANJA HAIGA DAR BILA KUTAKA

Na Musa Mateja
Wiki hii haikuwa njema kwa rapa mdogo wa Kibongo, Aboubakar Abdulaziz Chende ‘Dogo Janja’ baada ya Rais wa Manzese ambaye ni kiongozi wa Kruu ya Tip Top Connection aliyekuwa akimlea, Hamad Ally ‘Madee’ kumtimua Bongo, Risasi Jumamosi linakudondoshea ilivyokuwa.
Tukio hilo lililotokea Juni 13, mwaka huu baada ya Madee kupokea malalamiko kuwa Dogo Janja ameacha shule akiwa kidato cha pili katika Sekondari ya Makongo, Dar huku akidai kuwa anataka kwenda kusoma mkoani Arusha alikokulia.
Mbali na kukacha skonga, Madee alisema Dogo Janja alikuwa akijihusisha na mambo mabaya kinyume na makubaliano na wazazi wake waliomkabidhi amlee.
Dogo Janja alionekana akipunga mkono kwa mashabiki wake kwenye Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo, Dar akiwaaga kwa kusema: “Kwa heri Bongo, naenda zangu Ngarenaro (Arusha) kunywa chai na karoti lakini muda siyo mrefu nitawaibukia.”
Wakati akielekea kwao Arusha, Dogo Janja aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa BBM:
“Madee kweli kanisaidia kwa namna moja au nyingine kunileta Bongo ila kuna mapungufu ambayo pia kwake hawezi kuyafahamu na anakoelekea nahisi si pazuri, ilifikia kipindi hadi akawa ananinyang’anya simu na kutumia watu meseji za kunichonganisha.
“Nahisi uvumilivu kunishinda kutokana na habari zinazoongelewa na kaka yangu Madee, maana anachosema mimi nikisema kwa watu ataumbuka tu.
“Tangu anichukue kwetu na kuanza muziki sijawahi kupewa fedha taslimu zaidi ya Sh. laki 3 na siku zingine kuishia elfu 50.
“Madee alikuwa hana nia nzuri na mimi na nimegundua alikuwa ananisaidia kimuziki ili afaidike yeye, maana hapa naenda Arusha, akaunti yangu ina elfu 25 tu, halafu huwezi kuamini Madee katoa elfu 20 tu ya nauli, yaani kaniangusha sana na wala sikutegemea atanifanyia hivyo.”
Dogo Janja aliyewika na ngoma ya Anajua huku kukiwa na madai kuwa anataka kujiunga kwenye kundi fulani la muziki Bongo, aliwahi kuripotiwa kutoroshwa na mademu usiku jambo lililomkasirisha Madee lakini baadaye walimalizana.

No comments:

Post a Comment