Monday, June 18, 2012

DOGO JANJA HAIGA DAR BILA KUTAKA

Na Musa Mateja
Wiki hii haikuwa njema kwa rapa mdogo wa Kibongo, Aboubakar Abdulaziz Chende ‘Dogo Janja’ baada ya Rais wa Manzese ambaye ni kiongozi wa Kruu ya Tip Top Connection aliyekuwa akimlea, Hamad Ally ‘Madee’ kumtimua Bongo, Risasi Jumamosi linakudondoshea ilivyokuwa.
Tukio hilo lililotokea Juni 13, mwaka huu baada ya Madee kupokea malalamiko kuwa Dogo Janja ameacha shule akiwa kidato cha pili katika Sekondari ya Makongo, Dar huku akidai kuwa anataka kwenda kusoma mkoani Arusha alikokulia.
Mbali na kukacha skonga, Madee alisema Dogo Janja alikuwa akijihusisha na mambo mabaya kinyume na makubaliano na wazazi wake waliomkabidhi amlee.
Dogo Janja alionekana akipunga mkono kwa mashabiki wake kwenye Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo, Dar akiwaaga kwa kusema: “Kwa heri Bongo, naenda zangu Ngarenaro (Arusha) kunywa chai na karoti lakini muda siyo mrefu nitawaibukia.”
Wakati akielekea kwao Arusha, Dogo Janja aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa BBM:
“Madee kweli kanisaidia kwa namna moja au nyingine kunileta Bongo ila kuna mapungufu ambayo pia kwake hawezi kuyafahamu na anakoelekea nahisi si pazuri, ilifikia kipindi hadi akawa ananinyang’anya simu na kutumia watu meseji za kunichonganisha.
“Nahisi uvumilivu kunishinda kutokana na habari zinazoongelewa na kaka yangu Madee, maana anachosema mimi nikisema kwa watu ataumbuka tu.
“Tangu anichukue kwetu na kuanza muziki sijawahi kupewa fedha taslimu zaidi ya Sh. laki 3 na siku zingine kuishia elfu 50.
“Madee alikuwa hana nia nzuri na mimi na nimegundua alikuwa ananisaidia kimuziki ili afaidike yeye, maana hapa naenda Arusha, akaunti yangu ina elfu 25 tu, halafu huwezi kuamini Madee katoa elfu 20 tu ya nauli, yaani kaniangusha sana na wala sikutegemea atanifanyia hivyo.”
Dogo Janja aliyewika na ngoma ya Anajua huku kukiwa na madai kuwa anataka kujiunga kwenye kundi fulani la muziki Bongo, aliwahi kuripotiwa kutoroshwa na mademu usiku jambo lililomkasirisha Madee lakini baadaye walimalizana.

BABY MADAHA SASA HATARI


Baby Madaha akiwa na 'baby boy' wake mpya Slim.
Na Erick Evarist
BAADA ya kufichaficha sana, hatimaye staa wa muziki na filamu Bongo, Baby Joseph Madaha amenaswa na mwanaume ambaye inadaiwa ndiye usingizi wake kwa sasa.
Baby alinaswa na mwanaume huyo aliyefahamika kwa jina moja la Slim hivi karibuni maeneo ya Mwenge jijini Dar wakiwa kimahaba zaidi ambapo chanzo chetu kilicho karibu na wawili hao kilidai kuwa, walianzana ‘long time’ kwa kuibia.
“Sasa hivi Baby kajiweka kwa Slim baada ya kutosana na Rupee, ndiyo maana akaona amtumie kwenye video ya wimbo wake mpya wa Nimezama,” kilidai chanzo hicho.
Katika kupata ukweli wa habari hizi, mwandishi wetu alimtafuta msanii huyo na alipopatikana alisema: “Eee, hapa ndiyo nimefika licha ya kufanya naye kazi katika wimbo wangu mpya wa Nimezama, lakini jamaa ni zaidi ya kufanya naye kazi aiseee…”

Friday, June 1, 2012

BIFU LA AUNT EZEKIELI NA RAY LIMEISHA





BIFU la muda mrefu lililokuwepo kati ya wasanii wa filamu, Aunt Ezekiel, Steven Mangere ‘Nyerere’ na Vincent Kigosi ‘Ray’ limezimika baada ya mastaa hao kukaa na kuamua kumaliza tofauti zao.
Akizungumza na Ijumaa hivi karibuni katika Pub yake iliyopo Mwananyamala jijini Dar, Aunt alisema bifu hilo lililowafanya kutoshirikiana katika mambo ya kimaendeleo kwa muda mrefu lilikuwa likiwaathiri sana hivyo wakaamua kukubali yaishe.
“Unajua kifo cha Kanumba ndicho kilichotufanya sisi waigizaji tuwe kitu kimoja na kumaliza tofauti zetu ndiyo maana unamuona Ray na Steve wako hapa kwenye Pub yangu kuonyesha ni jinsi gani tunaungana mkono katika masuala ya maendeleo na si kuwekeana chuki zisizo na maana,” alisema Aunt.

USIKU WA SUGU NA MAKAMUZI MAZITO



WAKATI maandalizi ya shoo bab’kubwa ya muziki wa Hip Hop iliyopewa jina la Usiku wa Sugu, yakiwa yameshakamilika, wabunge kibao, bila kujali itikadi za vyama vyao wameahidi kujitokeza kumsindikiza mbunge mwenzao, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ atakayeongoza shoo hiyo ndani ya Ukumbi wa Dar Live, Mbagala Zakhem.
Akizungumza na Ijumaa kwa njia ya simu kutokea nchini Switzerland alikoenda kujifua sambamba na kufuatilia fursa za maendeleo kwa wananchi wake, Sugu atakayekamua na Profesa Jay na Juma Nature, aliwataja wabunge watakaomsindikiza Jumapili hii (Juni 3, 2012) kuwa ni Ester Bulaya, Idd Azzan, Amos Makala ambaye pia ni Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Zitto Kabwe, Freeman Mbowe, John Mnyika na wengine wengi.
“Tumeamua kumsindikiza Sugu katika shoo ya Dar Live bila kujali itikadi zetu kwa sababu anatuwakilisha wabunge wote. Kizuri zaidi kilichotufurahisha ni kwamba mapato yatakayopatikana ameahidi kuyatumia kutunisha mfuko wa elimu jimboni Mbeya.
“Tunaamini wanafunzi walioshindwa kuendelea na masomo kutokana na ukosefu wa karo, watalipiwa na shoo ya Usiku wa Sugu, kwa kweli ametufurahisha sana, lazima tumuunge mkono Jumapili hii,” alisema mbunge mmoja wa chama tawala kwa sharti la kutochapisha jina lake gazetini.